Wakati mwingine ninakasirishwa kazini au kwa watu wengine ambao wamekuwa marafiki zangu kwa kipindi kirefu. Hata ninaporudi nyumbani, ninapokutana na mke wangu tu huwa ananiuliza, “Mume wangu! Leo haupo sawa, tatizo nini?”
Wakati mwingine ninamficha kwamba nilikuwa poa lakini kila anaponibana, najikuta nikimwambia ukweli nini kimetokea. Sipendi kumuona akikasirika au kuhuzunika, ninapenda kumuona akiwa na furaha.
Veneranda! Ni mwanamke wa kipekee kwangu, alinipenda toka kipindi kile nikiwa masikini huku yeye akiwa ametoka katika familia yenye uafadhali kifedha. Hakuangalia fedha, hakuangalia umasikini, kitu pekee alichokuwa akikisikiliza ni moyo wake, ulisema nini juu yangu.
Kila ninapokaa naye, huwa ninamuuliza, alinipendea nini mimi masikini ambaye nilidharaulika sana lakini jibu lake kila siku lilikuwa ni kwa sababu mapenzi aliyokuwa nayo kwangu hayakuwa na mipaka.
Mke wangu Veneranda aliumbwa kwa ajili yangu, kila ninapomwangalia, huwa sijiulizi kumwambia ninampenda, amekuwa mtu wa tofauti kwangu, ninapokuwa na huzuni, ananipa furaha, ninapokata tamaa, ananitia moyo na kusonga mbele.
Mafanikio niliyokuwa nayo, mbali na Mungu, mke wangu Veneranda amechangia kwa sehemu kubwa. Nilipokuwa nikiungua jua kwa ajili ya kutafuta habari mitaani, niliporudi nyumbani, alinifariji na kuniambia kwamba safari imeanza na hivyo sikutakiwa kukata tamaa.
Kijana, mwanaume kwa mwanamke, unapofanya uamuzi wa kumuoa msichana au kuolewa na mvulana, fanya uamuzi ulio sahihi.
Wengine huziona ndoa zao kuwa chungu kwa sababu hawakufanya uamuzi sahihi.
Kijana, mwanaume kwa mwanamke, unapofanya uamuzi wa kumuoa msichana au kuolewa na mvulana, fanya uamuzi ulio sahihi.
Wengine huziona ndoa zao kuwa chungu kwa sababu hawakufanya uamuzi sahihi.
Wakati mimi ninasema kwamba kila ninapokuwa ofisini ninatamani kurudi nyumbani ili nimuone tena mke wangu nifarijike, kuna wengine hawataki hata kwenda nyumbani, wanatamani wahame nyumbani kwani wawenza wao wamekuwa miba mikali maishani mwao.
Huwezi kumuona msichana leo, ukasema kwamba unataka kumuoa, au umemuona mvulana leo na unataka kuolewa naye. Bado una muda wa kuzoeana naye ili baadae mtengeneze familia iliyo bora.
Ninapenda kuongea na vijana kuhusu maendeleo katika kufanya biashara yaani kujiajiri na hata kuzungumza kuhusu mahusiano yao. Hivi ni vitu viwili ambavyo hutegemeana.
Unaweza ukawa unafanya biashara inayokupa fedha nzuri lakini kama una mahusiano mabaya na mume wako au mke wako, bado fedha zitaonekana si kitu.
Hutakiwi kuingia katika ndoa kisa marafiki zako wote wapo kwenye ndoa, hautakiwi kuingia kwenye ndoa eti kisa umechoka kufua na hivyo unataka kufuliwa.
Kuna wengine huingia kwenye ndoa kwa kusema kwamba sasa mambo ya kukaa vichochoroni na wanawake kutakwisha au hatokuwa na wasiwasi katika kufanya tendo la ndoa.
Nisikilize rafiki yangu, siku ina masaa ishirini na nne, tendo la ndoa huchukua si zaidi ya saa moja, au tuseme limechukua masaa mawili kwa siku, kwa hiyo yanabaki masaa ishirini na mbili. Je, ndani ya masaa ishirini na mbili mtakuwa mnafanya nini?
Hapo ndipo kunapokuwa na mapenzi ya dhati, katika hayo masaa ndiyo kunakuwa na kujaliana na kusikilizana na mambo mengine kama hayo, kwa hiyo basi, kufanya tendo la ndoa linaweza kuchukua 2.00% katika maisha ya kila siku.
Hatuoi kwa ajili ya kufanya tendo la ndoa, hatuoi ili tufuliwe, na hatuoi li tupikiwe, ila tunaoa kwa sababu tuna mapenzi ya dhati na kuhitaji nguvu ya watu wawili katika maisha yetu ili tufanikiwe.
1 comment:
Mashaallah ujumbe mzito na mzuri sana kutoka kwako kaka ,Mwenyezi Mungu akubariki na awabariki wote walio katika ndoa na wanaotarajia ndoa.
Post a Comment