Mjadala……. Haki Ya
Kuzaliwa Ya Watanzania Ughaibuni
Taifa letu likiwa katika mpito na wakati mgumu wa kuandika rasimu ya katiba mpya ya watanzania, hatuna budi kuweka kando itikadi zetu za kisiasa, tofauti za kiimani na hata maslahi binafsi ili tuungane katika kutafuta katiba itakayokidhi mahitaji yetu ya sasa na ya vizazi vijavyo.
Katika
mchakato huu, inatubidi tuwe makini na wakweli katika kujadili hatma na haki ya
kuzaliwa ya ndugu zetu ambao wanaishi ughaibuni. Lazima tuwajumuishe na kuwapa
haki zao za msingi; haki ya kuzaliwa katika ardhi ya Tanzania ambayo
ni zawadi kutoka kwa mwenyezi Mungu. Hii ni haki ambayo kamwe haiwezi
kubatilishwa na mamlaka ya aina yeyote wala haiwezi kutenguliwa na binadamu
yoyote. Ni kujidanganya kudai kwamba waliochukua uraia wa kigeni warudi
Tanzania kama wageni.
Kwa makusudi
kabisa, nimeamua kuchokonoa huu mjadala wa haki ya kuzaliwa nikiwa na sababu
nyingi za manufaa kwa taifa letu; ya msingi ikiwa ni sababu ya kiuchumi na
hatma ya taifa letu. Jamii ya watanzania wanaoishi ughaibuni ni hazina adimu ya
rasilimali watu wanaohitajika katika maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii
ya Tanzania.
Ni kundi
lenye uwezo mkubwa wa kiuchumi ambao lazima tuwakumbatie. Mheshimiwa Rais
Jakaya kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waheshimiwa Dr. Wilibrod Slaa,
Freeman Mbowe, Bernard Membe, wote, kwa kipindi kirefu wameunga mkono haki ya
kuzaliwa ya watanzania wanaoishi ughaibuni kupata haki zao za msingi za kurudi
katika ardhi yao ya kuzaliwa bila masharti wala vikwazo vya aina yoyote
Bila shaka
wapo wanasiasa wenye ajenda zao binafsi ambao wamekuwa kikwazo kikubwa katika
kuwazuia wazawa wa Tanzania wanaoishi ughaibuni kupata haki sawa katika katiba
mpya. Siwezi kuwalaumu, kwani pengine wengi hawana uelewa wa faida ambazo
zitapatikana kwa kuwapa ndugu zetu waliozaliwa Tanzania haki ya kushiriki
katika ujenzi wa taifa.
Mjadala huu
tuaouanzisha lazima uweke katika mizani faida na athari za kuwapa watanzania
haki yao ya kuzaliwa na hatimaye kupata uwiano ambao utakidhi na kujibu maswali
mazito ambayo ndio chanzo cha vikwazo vilivyopo kwa sasa.
Wiki chache
zilizopita, Blogger-mwanasiasa mmoja nchini Tanzania alitoa shutuma dhidi ya
watanzania wajulikanao kama wana Diasapora wanaodai haki zao za kuzaliwa katika
ardhi ya Tanzania, huku akisahau kwamba yeye mwenyewe alikuwa mwana Diaspora
kwa miaka takribani thelathini. Hata kama alikuwa na uraia wa nchi thelathini,
mwisho wa siku alirudi katika ardhi aliyozaliwa yaani, Tanzania. Nina imani
kwamba anao wanafamilia ughaibuni ambao ndoto yao kubwa ni kutambulika kama
watanzania wenye haki zote ambazo kila mzawa anazo.
Katika
tafsiri isiyo rasmi ni kwamba amewatosa ndugu zake. Warudi Tanzania wasirudi
siyo tatizo kwake. Tofauti na mategemeo ya wengi, huyu blogger alitegemewa kuwa
mstari wa mbele kuhamasisha na kutetea haki za kuzaliwa za watanzania wanaoishi
ughaibuni.
Huyu blogger
ndio picha kamili ya wanasiasa ambao mara nyingi hutafuta nafasi za kupiga
picha na wanadiaspora pindi wanapotembea nchi nyingine ambako kuna watanzania. Wanasiasa
hawahawa watakuwa mstari wa mbele kujipanga uwanja wa ndege kuonyesha huzuni na
huruma na hata kumwaga machozi ya kinafiki pale majeneza ya wana Diaspora
yanaporudishwa katika ardhi yao ya kuzaliwa huku wakiwanyima haki zao za
kuzaliwa wanapokuwa hai.
Wengi wa
watanzania waliomba uraia wa nchi nyingine siyo kwamba hawalipendi taifa lao,la
hasha! Wengi ni wazalendo waliolazimika kuchukua uraia wa nchi nyingine ili
kupata ahueni kutokana na ugumu wa maisha unaowakabili mamilioni ya watanzania.
Wengine walitafuta vibali vya kuishi ili wapate elimu ambayo Tanzania
isingeweza kuwalipia.
Badala ya
kutafuta chimbuko la tatizo au wazo fulani, ni desturi yetu kama jamii kwa mjumbe
kusulubiwa na hata kuuwawa ili kuliua wazo au jambo linalotishia maslahi ya
wachache. Kumshambulia John Mashaka mathalani, hakutaweza kamwe kuliua swala
ambalo wakati wake umewadia. Binafsi nimeamua kubaki na uraia wangu wa
kitanzania licha ya kuwa na nafasi ya kuchukua uraia wa nchi nyingine. Kubwa ya
yote, ninajikita kuanzisha huu mjadala ili kuitetea Tanzania na rasilimali zake
hasa rasilimali watu.
Kama taifa,
tunawahitaji ndugu zetu wenye taaluma mbali mbali waliotapakaa kote duniani na
hata kufikia hatua ya kuchukua uraia wa nchi nyingine. Napigania watanzania
milioni 45 nikizingatia faida za kiuchumi, kisiasa, kijamii ambazo zinapatikana
na rasilimali watu wenye asili ya kitanzania. Wazawa wanaopigania haki zao za
kuzaliwa pamoja na vizazi vyao.
Ni muhimu
hawa wanasiasa wakakumbushwa kuhusiana na maamuzi yao ya kuwatenga watanzania
walio nje ya nchi, hususan kuwanyima haki zao za kuzaliwa. Inabidi wakumbushwe
kwamba, wazaliwa wa Tanzania wanaoishi ughaibuni wana ndugu zao Tanzania, ambao
ndio wapiga kura wao. Na ikiwa wanaamua kwa makusudi kuwatenga, basi kundi hili
maarufu kama Diaspora watumie uwezo wao, ushawishi wao na mbinu zote walizo
nazo kuwaadhibu wanasiasa wanaozuia haki zao za kuzaliwa
Pengine
niwakumbushie viongozi wa jumuiya za watanzania popote walipo duniani kwamba
haki haiombwi. Haki inadaiwa, na asiyeweza kudai haki yake na hata kuiona haki
yake kama zawadi au upendeleo fulani basi huyo amepoteza haki yake ya kuishi.
Viongozi wa jumuiya
za watanzania ughaibuni hawana budi kuonyesha uwezo wao wa kuongoza kwa kuwa
mstari wa mbele wakiwahamasisha watanzania waliotapakaa duniani kudai haki zao
za kuzaliwa. Inabidi wapaze sauti zaidi ili viongozi wetu walioweka pamba
masikioni wasikie madai yao. Mashabiki wa CCM ,CUF, CHADEMA na wengineo wote
wataathirika sawa. Kwa maana hiyo, vita hivi
havina mipaka, ni vita vya watanzania wa matabaka yote. Wana diaspora lazima wawe na mshikamano kama
watanzania.
Mungu
Ibariki Tanzania
John
Mashaka..
1 comment:
mashaka john, naomba mungu anipe uhai kuishi na kumuona mwanao. kweli umebarikiwa na kipaji cha kipekee. Amina
Post a Comment